Swahili quotes

Saturday, June 28, 2014

THE FAKE PRESIDENT/Rais Feki sehemu ya 1

Mtu yeyote anaweza kukua, kujifunza na kuwa Rais. Lakini, si kila Rais anaweza kufanya, kusababisha mabadiliko na mapinduzi makubwa kiuchumi,kijamii na kisiasa. Kiti cha Urais; ni kwaajili ya mtu maalumu mwenye tabia iliyotukuka na mtu wa watu, tabia kubwa,mgumu, mwenye uwezo mkubwa kiakili, maono makubwa, msimamo mkali,mzalendo na mwenye njaa ya mabadiliko asiyeendeshwa na watu wala matukio. Ni kwa mara ya kwanza Tanzania inampata Rais mwenye uwezo mkubwa uliotukuka. Mwenye maono makubwa . Mwenye hekima. Mwenye upendo wa dhati. Mzalendo wa kweli. Jasiri. Mtu wa watu.  Mh. Kennedy P. Kyando; rais mpya aliyeshinda kwa kishindo kupitia chama cha upinzani kiichwacho people's welfare party(pWp).
Siku ya kuapishwa kwake. Anasimama. Wananchi wote wanashangilia;

"People's"
"welfare"
"peoples"
"welfare"
Chama tawala kilichopita kimeangushwa. Ni historia mpya haijawahi kuandikwa Tanzania. Mhe. Kennedy; anatabasamu na kuanza hotuba yake; 



"Asanteni sana....
Ndugu wananchi. Hii ni siku kubwa ya kitaifa,najua yapo mengi mnatarajia kutoka kwangu. Huu ni muda wangu. Muda wa kuonyesha uwezo wa serikali yangu. 

Ndugu wananchi ninajua sababu ya kura zenu. Ninaweza kusema; malipo ya kura zenu ni kusababisha maono ya picha kubwa niliyonayo kuhusu Tanzania yetu kwa kujenga upya uchumi wa nchi yetu . Kurudisha rasilimali za watanzania kwa watanzania. Kurudisha upendo,amani, umoja na siasa safi si tu kwa watanzania pekee bali kwa dunia nzima; na katika vizazi vyote.

Tanzania ni taifa kubwa lenye uwezo wa kuongoza ulimwengu kisiasa,kiuchumi na kijamii. Tangu tupate uhuru; sijui labda hatukubahatika kupata kiongozi aliye tayari kujitoa sadaka kusimama mpaka mwisho kujenga na kusababisha maono yake. Wengi waliishia njiani. Lengo langu si kulalamika na kuwalaani viongozi waliopita; bali nataka tuijenge Tanzania upya. Imani yangu inaniambia kuwa Tanzania itapona. Magonjwa yote ya kimaskini,rushwa,uoga,ujinga na katiba yake yote yatapona.
Sera zangu; zimebeba nguvu na mipango madhubuti ya kusababisha mambo makubwa Tanzania.

Ndugu wananchi, ninayo maono makubwa. Ninaiona Tanzania mpya. Tanzania kubwa.Natambua kuhusu mapungufu ndani ya katiba yetu. Katiba ni moyo wa nchi yetu. Ni biblia au quran ya serikali; lakini inaweza kubadilishwa na kuboreshwa kimanufaa kwa maendeleo ya nchi yetu na kwa matakwa ya wananchi. Katiba si kwaajili ya chama; ni kwaajili ya wananchi. Lazima; tuhakikishe inasimama kwaajili ya wananchi. 

 Ndugu watanzania; natamani Tanzania mpya.Safari yangu ya uongozi inategemea sana msaada wenu. Hii serikali; ni yenu. Ni mawazo yenu. Mafanikio yake; yatatokana na mawazo yenu. Ninaamini katika uwezo wenu; na lazima serikali isimame kwaajili yenu. Serikali isiyosimama kwaajili ya wananchi; ni Serikali feki, ni genge la wezi na majambazi. Siwezi kuruhusu serikali ya aina hiyo. Hivyo basi; ni muhimu kubadili vipengele kadhaa vya katiba yetu; na hiyo itakuwa kazi yangu ya kwanza nitakayoanza leo. Nitapigana kwa uwezo wangu wote, roho yangu yote na akili yangu yote. 
 
 Sipo tayari kuruhusu mwanadamu yeyote; nchi yoyote izuie ndoto kubwa ya kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha mafanikio, amani na upendo. Nipo tayari; kufa hata leo kuliko kuzuiliwa  kusababisha ndoto hiyo"



Mhe. Kennedy alimaliza hotuba yake; na kuanza kushangiliwa......
 "Peoples"
"Welfare"
"Peoples"
"Welfare"

Kila mtanzania; alikuwa akishangilia. Tanzania imepata Rais wa kweli. Mhe. Kennedy alipogeuka; kuelekea kwenye kiti chake; ghafla. alipigwa risasi kichwani na mwenyekiti wa chama chake cha People's welfare party; Mhe. Albert Komba. Hii kitu gani tena? Viongozi wote wa people's welfare party; waliokuwa karibu na Mhe. Albert  walikimbia na kwenda mbali  kuokoa maisha yao. Walinzi watano wa Mhe. Rais; wakiwa wamevaa suti nyeusi walimfuata Mhe. Rais; kwa spidi kali ili kuokoa maisha yake. Walikuwa wamechelewa. Mhe. Kennedy; yupo chini. Walinzi wamemzunguka; ili kuzuia risasi nyingine.
Mke wa Mhe. Kennedy Pius Kyando; Mama Edda Kennedy Kyando; ambaye alikuwa amesimama pembeni ya kiti cha Mhe. Rais hakuamini macho yake. Hii kitu gani tena? Wananchi walianza kukimbia kuokoa maisha yao. Siyo hali ya kawaida; na watanzania wengi hawajazoea maisha ya bunduki. Hiyo ilikuwa ni mshtuko kwao. Bado hali haieleweki. Askari watano; walimvamia Mhe. Albert kwa nyuma; akiwa bado ameshikilia bunduki yake. Hakuonyesha kujali wala kuogopa. Uwanja wa Taifa; haupitiki tena. Hali ni mbaya. Maafisa usalama walimzunguka Mhe. Rais; na kuzuia kusogelewa na watu. 
Baada ya dakika mbili; tayari gari la wagonjwa limeshafika uwanja wa Taifa. Ni nani ametoa taarifa ndani ya muda mfupi kama huo? Bado ni maswali yasiyo na majibu. Chama cha People's welfare kilianzishwa na maswahiba hao wawili mwaka 2005; Mhe. Kennedy na Mhe. Albert; iweje leo Mhe. Albert achukue maisha ya swaiba yake? Kuna siri gani imejificha? Bado haieleweki. Mhe. Rais aliingizwa ndani ya gari la wagonjwa; bado haieleweki kama amefariki au yupo hai.
Watanzania; bado wamechanganyikiwa. Bado hawaamini kitendo kilichotokea. Ni kwa mara ya kwanza Tanzania. Mtoto wa kike na pekee wa Mhe. Kennedy, Ms. Lilian Kyando; analia huku anakimbia kulifuata gari lililombeba baba yake. Mama Eda Kyando; amepoteza fahamu; wamama wanajitahidi kumpa huduma ya kwanza. 
Mhe. Rais alikimbizwa mpaka; Hospitali ya Mhimbili na kupelekwa kwenye chumba maalumu kwaajili ya operesheni. Waandishi wa habari; zaidi ya 500 wapo nje ya hospitali. Vyombo vya habari TV, radio vyote ni breaking news. Mhe. Rais yupo mahututi; madaktari wakubwa Tanzania wapo ndani ya chumba kuokoa maisha ya shujaa wa Tanzania. Mhe. Albert Komba; alifikishwa  kituo cha polisi kwaajili ya upelelezi zaidi. Akiwa kituoni; hakuonyesha kujali wala kuogopa; zaidi alikuwa akicheka kama kichaa. Swali; ni kweli ni kichaa au kuna nyuma ya pazia?


ITAENDELEA JUMAMOSI IJAYO......
TSL Books-Geophrey Tenganamba.


.

No comments:

Post a Comment