Swahili quotes

Thursday, June 26, 2014

SIRI INAYOANGAMIZA SEHEMU YA PILI.


SIRI INAYOANGAMIZA SEHEMU YA PILI.


"Beee mama" Helena aliitika na kumwacha Steve bado ameduwaaa chumbani kwake. Alipofika sebuleni alikuta mama yake amesimama, mkono wake wa kulia umeshikilia kitambaa cha kusafishia vyombo.
"Steve anafanya nini chumbani kwako?" Mama aliuliza. 
"aah! alikuwa anauliza kama kuna rafiki yangu yeyote alikuja jana"

Helena alijibu, mkono wake wa kulia ukiwa kichwani. 
"Anatafuta marafiki zako wa nini? Irene hamtoshi?" Mama aliuliza, na kukunja sura yake. 
"mmh" Helena hana la kusema. Mama akaendelea. 
"Tena inabidi aoe, ninahitaji mjukuu  atakayebeba jina la ukoo wa Mtambaji na siyo; vinginevyo". 
Steve alitoka chumbani kwa spidi. Helena na mama yake wamesimama. 
"Mama shikamoo". 
"Marhaba , ehee unatafuna nini chumbani kwa dada zako". Mama hakutaka kupoteza muda. Steve alitulia kidogo; ili kupanga mawazo yake kichwani. Bado akili yake ipo vitani. 
"Mama, jana hukuona mgeni yeyote usiku hapa nyumbani?". 
Mama alicheka,kicheko cha masikitiko. Helena naye akaanza; 
"Mama hata mimi simwelewi". 

Steve hakutaka kuendelea na maongezi yale. Aliondoka na kwenda moja kwa moja hadi jikoni; aliko mfanyakazi wa ndani. Nyumba yao ilikuwa kubwa; na ilikuwa inajaa wageni kila siku. Wadogo zake watatu wote; Leonard, Helena na Prisca; walikuwa wanasoma. Ilikuwa ni vigumu kuhudumia nyumba bila mfanyakazi wa ndani. Na mama tayari uzee ulikuwa umeanza kumnyemelea. Hivyo Tina; ni mfanyakazi wa ndani ambaye ni dada mwenye umri mkubwa zaidi ya miaka 27. Alipofika jikoni; bila salamu akauliza; 
"Jana hujaona mgeni yeyote hapa nyumbani? Msichana; mweupe anaitwa Nas, rafiki yake Helena?"

"Kaka, jana hatujapokea mgeni yeyote. Tumeshinda na mama muda wote. Helena amerudi saa nne usiku peke yake.Na mimi nilikuwa wa mwisho kulala, nilikuwa naangalia filamu uliyoleta". 

Steven hakuamini alichosikia, akaenda hadi chumbani kwa mdogo wake Leonard ambaye bado alikuwa amelala
“Leornad bado umelala?, hebu amka".  Leonard aliamka na kusalimu   
"Shikamoo kaka"
Masikio yake, hayakuweza kusikia salamu yake. Akiwa ameshikilia mlango; akauliza
"eti jana hujaona mgeni yeyote wa kike?"
Leonard alijibu; 
"Hapana kaka, kwani ni nani huyo? ".

 Steven hakutaka kuendeleza maongezi. Aliondoka na kwenda chumbani kwake. Mdogo wake akashukuru Mungu; kuona kaka yake ameondoka bila kumfokea kwa kuchelewa kuamka.Akiwa chumbani; alifungua simu yake ili kusoma meseji ya simu yake. Alishtuka kukuta meseji aliyotumiwa imepotea. Wasiwasi ulianza kutawala mawazo yake. Ndipo alipoamua kuondoka. Nikifika kazini, nitasahau kila kitu. Alipofika sebuleni; mama na Helena bado  wanaongea. 
Aliaga ; "Sasa mimi natakiwa kuwahi kazini"
Mama akaita "Steve, hebu njoo".
Alimsogelea "Mama nachelewa, nina kikao saa moja jioni na wafanyakazi wangu"
"Sawa, wewe ni bosi. Unaweza kuchelewa, au hata kuahirisha kikao. Nataka uniambie umetokewa na nini jana usiku?"
Steve akatabasamu. "Mama, hakuna kitu. Naomba niwahi. Helena; ada yako nimeshalipa".
Hakutaka kuyasema yaliyotokea kwa ndugu zake. Ni aibu. Aliondoka kwa haraka; mama akabaki anaita "Steve....Steve...". Alifika mpaka kwenye gari yake; aina ya Prado. Lililokuwa limepakiwa nyumba ya nyumba yao na kuondoka.
  
Alifika kazini muda wa saa moja na dakika kumi. Na kusalimiwa na wafanyakazi wake wa kampuni ya Mtambaji Media. Ni kampuni ya matangazo, kutengeneza filamu na kusambaza, ushauri wa biashara na uchapaji. Steven alikuwa ni muigizaji maarufu na mkurugenzi wa kampuni hiyo. Ilipofika saa moja na nusu walianza kikao. Tofauti na kawaida yake, hakuwa na furaha kabisa. Wafanyakazi waliogopa, wakahisi labda ana matatizo nyumbani lakini hataki kuyasema. Kila akikumbuka yaliyotokea jana usiku; alijikuta anajiongelea.
Mkurugenzi msaidizi akauliza; 
"Bosi, vipi mbona hauko sawa leo?". 
"Niko poa, hebu hakikisha yametengenezwa mabango yote. Na kama ikiwezekana leo leo mkalipie manispaa ili yabandikwe". Alimaliza kikao; na kurudi ofisini kwake. Sekretari wake; Jasmin ni mcheshi sana. Alijitahidi kumchekesha bosi wake; na kuambulia majibu makavu.

Hata ilipofika muda wa chakula, alishindwa kula. Mawazo yake yalizidi uwezo wake wa kuyamudu. Jioni akiwa njiani kurudi nyumbani; kidogo apate ajali kutokana na mawazo yaliyokuwa yanaogelea katika kichwa chake. 

Alipofika nyumbani, alienda moja kwa moja mpaka chumbani kwake,akakuta chumba chake bado kinanukia pafyumu ya yule msichana. Ilizidi kumchanganya. Siku ilipita, kesho akaamuru chumba chake kisafishwe chote. Nguo zake zote zisafishwe ili kupoteza harufu ya pafyumu ya mwanamke huyo. Tina alifanya hivyo; akisaidiana na mdogo wake Prisca. Walifanya kulingana na maelekezo. Aliporudi kutoka kazini; alishangaa kuona harufu ya pafyumu ipo vilevile. Na ilizidi. Alimuuliza Tina kama wamepulizia pafyumu yoyote chumbani kwake; 
"Kaka, hatujapulizia pafyumu. Ni pafyumu yako. Ni nzuri sana". Ilimchanganya. Akaamua kudharau; na kujifanya hasikii. Wiki mbili zilipita, na kuanza kusahau yote; lakini harufu bado haijatoweka.  Ilipofika mwisho wa mwezi tarehe; 31/01/2001; muda wa saa tisa usiku; Steven akiwa amelala; alishtuka kukuta amekumbatiwa. 
Aliwasha taa. Alishangaa kumuona msichana yule amelala; usingizi. Tena anakoroma. Steven aliogopa sana, Akauliza kwa kutetemeka ; "wewe ni nani?" Hakujibiwa. Msichana amelala,yupo usingizini. Ilimpa shida, akiwa amesimama karibu na mlango, sauti moja inamwambia kimbia wakati sauti nyingine inamwambia mwamshe ujue ni nani. Alijikuta amesimama hajui afanye nini kutokana na kigugumizi cha maamuzi.
                     ITAENDELEA WIKI IJAYO...ALHAMIS IJAYO.
                      TSL books-Geophrey Tenganamba




No comments:

Post a Comment