Swahili quotes

Friday, June 27, 2014

MAISHA YANGU DUNIANI SEHEMU YA PILI

MAISHA YANGU DUNIANI. 
"Mahojiano kati ya Mimi na Mungu"
Simulizi ya uamsho. 
Kabla sijaondoka duniani niliishi maisha ya bora liende. Nilitumika na watu wenye ndoto kubwa kama spea ya trekta. Dini yangu, nilijivunia dini yangu na kupumbazika kwa majivuno. Wale waliotofautiana na mimi; niliwatenga na kuwahukumu kama Mungu. Sikujua ukweli. Sikujua kuwa yote niliyosoma. Yote yaliyokuwa kichwani mwangu yalikuwa ni upupu tu. Yaliniendesha na kunifanya niishi kama mashine isiyo na roho kwa ndani. Nilijikuta miaka yangu inakimbia tu; hakuna cha maana nilichofanya duniani.

Nilipofikisha miaka 89, Mungu akachukua uhai wangu. Nilipofika mbinguni sikuamini niliyoyakuta. Nilijuta.Nilijuta sana. Laiti kama ningejua ukweli; nisingeishi maisha niliyoishi. Nilipatwa hasira; kwanini Mungu alinileta duniani na kuniacha peke yangu wakati wa mateso? Maisha niliyoishi miaka 89 duniani yalikuwa ni ya dhiki na njaa. Kwanini mimi? Nilifunga ndoa yangu; nikiwa na miaka 35 lakini ndani ya ndoa ilikuwa ni migogoro na matusi; kwanini? Umaskini kwangu ulikuwa umegandamana kama damu ndani ya mwili wangu. Kila nilipojitahidi kujitoa nilishindwa. Watu wengine walikuwa wanafanikiwa mbele ya macho yangu; nilikosa nini kuishi maisha ya chini?
Nilijitahidi kuishi maisha kama nilivyoelekezwa na viongozi wangu wa dini; wazazi wangu na elimu yangu nikidhani kuwa labda nikija huku mbinguni nitapumzishwa na kuvikwa taji na kusahau mateso yote ya miaka 89 iliyopita duniani. Cha ajabu nilipofika huku mbinguni niliyoyakuta yamenipasua moyo. Kwanini? Kichwa changu kilikuwa kimejaa maswali yasiyo na majibu. Maswali ambayo ni Mungu peke yake ndiye mwenye majibu.
Niliwaona malaika wakizunguka zunguka katika  geti la mbinguni; akili ikaniambia nikaombe nikutanishwe na Mungu mwenyewe. Nataka majibu kwa Mungu mwenyewe na siyo mtume. Nilisogea mpaka kwenye geti; lenye rangi nyeupe. Mwanga wake uling'aa  kama mwezi usiku. Nikiwa nimesimama; nikasikia sauti nzuri za muziki. Sijawahi kusikia sauti nzuri kama zile katika maisha yangu. Malaika; hawakunijali hiyo ilinipa hasira zaidi; ghafla nikasikia sauti; 
"Mr. Anderson; huwezi kuruhusiwa kuingia mbinguni na mizigo yako. Huwezi. Watu kama wewe; wanadamu mlioshindwa kuishi duniani kwa kutumia hazina iliyowekwa ndani yenu kimanufaa kwa matakwa ya Mungu,hamstaili tuzo duniani na wala mbinguni. Hebu fikiria watoto kumi uliozaa na kuwaacha duniani wote ni vibaka. Ndoto na vipaji ulivyopewa hujatumia hata kimoja. Leo hii unataka uruhusiwe kuingia mbinguni; kwa kazi gani uliyofanya duniani? Hiyo ni mizigo yako. Ondoka hapa"

Hasira ilinipanda. Watu wote waliokuwa wanaingia; waliruhusiwa kulingana na kiwango cha matumizi ya hazina na uwezo wa kiroho siyo kidini uliyowekwa na Mungu ndani yao. Hakuna dini wala mdogo wake dini. Kumbe mbinguni hakuna dini? Nikakumbuka mbona kila siku nilikuwa mhudhuriaji mzuri wa ibada,Kazi na kutii sheria zote? Nilifuata amri zote na kutenda yote? Kwanini? Malaika akasikia mawazo yangu. Akajibu;
"Ni nani aliyekufundisha hayo? Na amri hizo ulizitoa wapi? Una uhakika gani zilikuwa ni amri za Mungu na siyo wanadamu? kwa msukumo upi? kwa malengo yapi? "
Malaika alizidi kunichanganya. Nikajibu ; 
"Ninataka kuonana na Mungu mwenyewe. Ninataka kumuuliza maswali. Ninataka majibu".
Malaika akajibu kwa tabasamu; 
"Sasa hata ukiuliza maswali na kujibiwa yatakusaidia nini wakati wewe huna maisha ; na huwezi kuruhusiwa kurudi tena duniani?"
Nikafikiria; nikajibu; "Nataka kuandika barua na kuituma duniani iitwayo; maisha yangu duniani. Kupitia barua yangu, labda watoto wangu na wanadamu wengine watapata ukweli na kuanza kuishi ukweli"
Malaika akauliza; 
"Wewe utafaidika nini?"
Nikatabasamu; nikashangaa kumbe hata uwezo wangu wa kufikiri kiroho ulikuwa mkubwa kuzidi malaika. Laiti kama ningejua; nisingeishi maisha niliyoishi. Nikajibu;
"Faida ya kweli ni matokeo ya kile unachotoa na si kile unachopata"
Malaika akacheka; "mbona ulipokuwa duniani hukuishi hivyo?"
Nikasema ; "Naomba niruhusu nikutane na Mungu tafadhali. Nipo tayari kwa chochote; lakini baada ya kujua ukweli. Ukweli kutoka kwa Mungu mwenyewe na si kwa mtu mwingine. Nilipokuwa duniani, nilipumbazwa na watu; nikawasikiliza watu na kudharau sauti ya ukweli. Sauti ya Mungu. Sitaki kurudia kosa hilo tena"

Malaika; alishtuka. Maneno yangu yalimwingia. Akaamua kufungua geti.

 Nilipoingia ndani; mbinguni nilishtuka. Nikagundua kuwa mbinguni siyo sehemu; mbinguni ni hali chanya wazungu wanaita positive state. Zaidi ya hayo;nikashangaa kuona mimi ni hali niliyekuwa naishi ndani ya mwili wangu nikiwa duniani. Nikakumbuka usemi wa UFALME WA MUNGU UPO NDANI YENU. Laiti kama ningejua; nisingekubali mwili wangu utawale maisha yangu na kusahau hali-uwezo wa kiungu ndani yangu. Nilitembea kidogo na kuona malaika wanaimba; wanacheza kama watoto wadogo. Nikakumbuka kuwa; kama ningeishi roho na hali chanya kama  mtoto huku napigania malengo yangu nisingekosa raha na zaidi ningefikia ndoto zangu. Nikatembea kidogo; nikakiona kiti cha enzi, Nguvu kubwa inayoongoza isiyopimika ikaonekana.Ikawaka na kuamsha nguvu na hali chanya ndani yangu. Ni Mungu. Tayari maswali yangu yakaanza kupata majibu.Sauti ikasikika; 

"Una uhakika kweli unataka majibu ya maswali yako au una jaribu jaribu tu kama ulivyokuwa duniani?"

"Nina uhakika Mungu wangu. Nina ukakika; kwasasa sibahatishi. Nataka ukweli" Nilijibu kwa kujiamini. 
Mungu akajibu "Okay, nipo tayari kujibu maswali yako"

Nikauliza "Mungu wangu, mbona nilipokuwa duniani hukunisikia na wala kuwa karibu yangu kama leo?"

"Siyo kweli. Kila siku. Kila siku nilikuwa naongea na wewe. Muda wote. Mimi ni Mungu ninayeongea na kila mwanadamu, kila siku na kila wakati.Nipo karibu na wanadamu zaidi ya ukaribu huu. Tatizo; wengi wana masikio lakini hawanisikii. Wapo tayari kusikiliza uongo kutoka kwa wanadamu wengine kuliko sauti yangu kutoka mioyoni mwao"

Jibu lake lilinipa shida kidogo. Kumbe Mungu alikuwa karibu yangu. Mwanzoni nilidhani Mungu yupo MBINGUNI mbali na mimi kumbe siku zote alikuwa ndani yangu akiongea na mimi siku zote,muda wote. Ikabidi niulize tena; 
"Mungu wangu, naomba unipe maelezo kwa undani kuhusu ukweli huu. Nimepanga kutuma ujumbe huu kwa wanadamu wote kupitia barua ya maisha yangu duniani"


 Mungu akajibu ; "Lugha. Watu wengi hawajui lugha yangu. Zipo lugha mbili tu duniani; lugha ya kimwili ambayo asili yake ni mwili na lugha ya kiroho ambayo asili yake ni mimi. Dini zenu zinaendeshwa na lugha ya kimwili. Na mengi mnayofundishwa ni kupitia lugha ya kimwili. Lugha ya maneno ni lugha ya kimwili. Wengi hawanisikii kwasababu kila siku wanasikia lugha ya maneno kupitia masikio yao ya kimwili na siyo lugha ya hisia kupitia masikio yao ya kiroho. Lugha yangu ni ya rohoni. Lugha yangu ni ya hisia; hisia chanya na picha. Ni lugha ninayoweza kuwasiliana na wewe kupitia wewe na siyo mtu mwingine. Ni lugha unayoweza kujua ukweli wa yote. Ukweli wa kweli haupimwi na uwingi wa maneno; au umaarufu wa mtu anayesema. Ukweli wa kweli hupimwa na jinsi unavyojisikia mwenyewe moyoni. Ulipokuwa duniani ulijidharau na kujiona mdogo, ukawapa madaraka wanadamu wengine waamue mfumo wa kufikiri kwako. Hisia zako na kusahau ukweli wa hisia kutoka moyoni mwako. Ukaishi maisha ya mkumbo; na kuamini uongo kutokana na uwingi wa watu wanaoamini uongo huo. Nakukumbusha tena, ukweli wa kitu haupimwi kwa uwingi wa watu wanaoamini ukweli huo; bali unapimwa kwa hisia za kweli zinazotoka moyoni mwako"

Nilibaki nimesimama. Nashangaa. Kumbe niliyofundishwa na kuaminishwa yana mapungufu. Uoga ukaanza kuniingia; ikitokea nimetuma barua hii duniani; wanadamu watanichukuliaje. Nikakumbuka kuwa mimi ni marehemu; hawawezi kunidhuru. Mwandishi nitakayemtumia kuandika barua hii; atapokelewaje? Watampiga mawe? Nikajipa moyo; mwandishi ni mjumbe tu. Mjumbe hauawi. Nikaanza kukumbuka mateso ya wanadamu duniani. Nikagundua kumbe wengi hawajui ukweli. Nikaendelea; 
"Mwanadamu afanyaje, ili aweze kusikia lugha ya picha na hisia  za ukweli wa kweli kutoka moyoni mwake?"

Mungu alitabasamu kidogo. Nikatabasamu pia. Akaendelea......

FUATILIA KISA HIKI CHENYE UKWELI WA KWELI KILA IJUMAA. SOMA KITABU HIKI UKIWA UMETULIA; KIMEBEBA UJUMBE UNAOWEZA KUAMSHA IMANI YA KWELI MPYA.
TSL BOOKS TANZANIA. Geophrey Tenganamba

No comments:

Post a Comment