Swahili quotes

Tuesday, July 1, 2014

Nikumbuke Mpenzi wangu sehemu ya tatu...

 NIKUMBUKE MPENZI WANGU...REMEMBER ME MY LOVE SEHEMU YA TATU

"narudia tena hampaswi kujua chochote kwa undani kuhusu huyu Dada"
Maneno ya dokta Adam yalizidi kunichanganya. Labda amechanganyikiwa. Kuna nini kinaendelea katika maisha yangu? Nimetokewa na nini? Ni nani amehusika katika ajari yangu? Ndugu zangu wako wapi? mume Wangu Osward yuko wapi? Baada ya maongezi yao'; Dokta Adam aliondoka na kuniacha mpweke tena. Walibaki wahudumu wawili Deborah na Frank na Dokta Michael. Baada ya dakika kadhaa nikasikia sauti ya Michael;
 "hakuna MTU yeyote aliyekuja kumuulizia mgonjwa huyu?"  Deborah akajibu "yaani huyu Dada toka aletwe hapa hospitali ni Dokta Adam pekee amekuwa akimhudumia kisiri. Na zaidi; tumeambiwa harusiwi mtu yeyote kuja kumuona wala kujua uwepo wake; hasa ndugu zake"


Frank akaongezea  "Huyu dada anatia huruma sana. Inaonyesha ameumizwa na mtu aliyekuwa akimwamini sana. Huwezi kuamini aliokotwa kutoka sehemu aliyotupwa kama mzoga. Binadamu hana utu kabisa. Sijui kama atatoka mzima"

Michael; akaguna na kuuliza ; " kwani ni kitu gani kimemtokea? Mume wake yuko wapi? Au ni kutokana na utajiri wake?"

Frank alitabasamu kwa sauti; akajibu " Yaani Michael; mkasa wa huyu dada una mengi yamejificha. Laiti kama ungemuona siku alipoletwa; usingeamini; alikuwa amelowa damu kama kuku aliyechinjwa". 
Mazungumzo yao yalinitia kichaa. Niliogopa sana. Kila kitu. Kila neno lililotoka katika midomo yao kwangu ilikuwa ni kitendawili. Maisha yangu yalikuwa katika giza la sintofahamu. Michael akasema;
"Sasa ninawaacha kidogo. Naenda wodi ya akina mama; kwaajili ya operesheni. Mwangalieni na zaidi kuweni makini; si mnamjua Dokta Adam?"
Wote walicheka; mlango ulifunguliwa na kufungwa. Michael aliondoka. Nilijisikia mpweke na mnyonge zaidi. Nilijisikia vibaya sana; kama nimetengwa. Kuondoka kwa Dokta Adam na Michael; kulinikosesha amani. Sikuwaamini wahudumu waliobaki. Nilijipa moyo na kusema; kama kweli Mungu yupo. Kama kweli Mungu ananipenda; hataniacha katika giza hili bila majibu wala sababu. Nitauona mwanga.Lazima nitauona mwanga. Nikasikia sauti ya Frank;
"Siwezi kuamini; hali aliyokuwa nayo huyu dada alikuwa si wa kufika mpaka siku ya leo"

Deborah; alitabasamu kidogo akasema;
"Kumbuka ni Dokta Adam; amefanya operesheni. Dokta Adam hajawahi kumpoteza mtu katika operesheni. Hata hivyo sidhani; kama atatoka mzima. Akibahatika kuamka; hawezi kuwa kama mwanzo. Uzuri wake wote kwaheri. Angalia miguu yake na mikono ilivyosagika. Huyu mtu aliyemfanyia unyama; ni zaidi ya shetani. Uso wake hautamaniki kabisa. Kichwa chake; jamani kama chapati ya maji. Yaani; ni bora ajitangulize mwenyewe mapema. Huwezi kuishi duniani na sura kama yake"

Maneno ya Deborah yalinitisha sana. Yaani nimeharibika? Mwili wangu umekuaje? Uso wangu umekuaje? Kama uzuri wangu umepotea; nitaonekanaje? Waandishi wa habari wanajua kuhusu kuharibika kwa sura ya Mkurugenzi wa Patricia Hotels & Apartments group? Nimekuaje mimi? Maswali yalinijaa kichwani bila majibu. Sikujua la kufanya zaidi ya kusubiri kitakachotokea. Nilijisemea moyoni mwangu; Mungu wangu sikia sauti yangu; popote kule uliko. Nikasikia sauti tena;

"Dada Deborah; natoka kidogo.Njaa itanitoa roho" Alikuwa ni Frank huku akitembea kwenda mlangoni.
Deborah akatoa sauti ya kelele na kali;
"Hey hey; kwahiyo unataka kuniacha peke yangu na huyu dada? Kikitokea kitu je; nitafanyaje peke yangu? Dokta Adam amesema; tusitoke. Nani anataka kubaki peke yake na huyu mtu anayetisha hivi?"
Frank akacheka;
"Acha uoga; hakuna kitu kitakachotokea. Ikitokea nibipu; nitakuja kwa spidi"
"Hapana..hapana...siwezi kubaki peke yangu. Chumba chenyewe kina giza" Deborah aliongea huku akimzuia Frank.
Frank alimbembeleza; na kuondoka.
Maongezi yao; yalinitia uchungu. Nilipatwa hasira. Mwili wangu umekuaje kiasi cha kuogopwa na wahudumu? Nilitamani nisimame niwapige makofi. Dunia kwangu ilikuwa ni giza. Mbingu ilikuwa mbali nami. Nilikuwa ulimwengu wa peke yangu. Ulimwengu wa upweke. Ulimwengu usiojali uwepo wangu. Deborah alibaki analalamika. Nikasikia sauti yake;
"Patricia..Patricia...jitahidi uamke au kama vipi tangulia kwa Mungu ili na sisi tupate nafasi ya kulala"

Nilijisikia vibaya. Nilikumbuka utajiri wangu wote. Maisha yangu yote niliyoishi. Watu wote niliowasaidia. Kaka yangu. Mume wangu. Rafiki zangu. Wote hawakuwepo. Nilikuwa peke yangu. Kama wangekuwepo labda wangenisaidia. Deborah alilalamika mpaka akaanza kusinzia. Niliumia sana. Nilijitahidi kuamka; lakini nilishindwa. Nikajiuliza hivi mimi nimekufa au nipo mahututi. Nipo ndani ya mwili wangu nimefungwa katika giza lisiloeleweka. Sijulikani kama nipo kuzimu au nipo ahera. Siwezi kufanya chochote zaidi ya kusikia sauti za watu waliokuwa ndani ya chumba cha operesheni. Deborah alianza kukoroma; na kuniacha peke yangu. Nikamkumbuka Dokta Adam; kama angekuwepo maneno yake yangenifanya nijione sipo peke yangu. Kila nilipojaribu kutikisa mwili wangu nilishindwa. Nikasikia sauti ndani ya akili; ndani ya kichwa changu. Ilikuwa ni sauti ya kiume; ni sauti inayofanana na sauti ninayoifahamu lakini siikumbuki;
"Patricia..Patricia huwezi kushindana na mimi"
Kupitia kichwa changu nikauliza;
"wewe ni nani? kushindana na wewe kivipi?"
Hii ilikuwa ni maajabu ya dunia. Maongezi yetu yalikuwa kupitia kichwa changu; na siyo mdomoni. Hii ni kwa mara ya kwanza; kwangu. Nikajiuliza au nimekuwa kichaa? sauti ikasikia mawazo yangu na kujibu;
"Wewe ni kichaa. Mpumbavu. Mjinga wa kutupwa. Kufaa...kufaa..kufa Patricia kufa unanikosesha raha"
Nilitishika sana. Nikajitahidi kujibu ;
"Siwezi kufa bali nitaishi. Mungu pekee ndiye atakayepanga lini nife. Wewe huna uwezo wa kutoa uhai wangu"
Nilitamani Dokta Adam arudi haraka ili japo nisikie sauti yake. Nilitamani mume wangu aje na kuniokoa na mtu nisiyemjua anayepigana nami kupitia kichwa changu. Niliogopa sana kwani nilikuwa katika giza; sioni kitu zaidi ya sauti kichwani. Nilijirusha lakini mwili wangu haukutikisika hata kidogo. Nikasikia tena;

"wewe ni kichaa. Wewe ni kichaa"
Nikajibu "mimi siyo kichaa ..mimi siyo kichaa..".
Ukweli sikujua ni kitu gani kinaendelea; nikajiuliza au mtu akiwa kichaa hupigana vita akilini na watu asiowajua kama mimi?  Nikasikia;
"Patricia...nitachukua mali zako zote. Na vitu vyote unavyovipenda. Ukiamka; hutaambulia chochote. Bora uchague kufa leo; kufaaaa"

ITAENDELEA JUMANNE IJAYO.....USIKOSE.
TSL Books-geophrey tenganamba.

No comments:

Post a Comment