Swahili quotes

Wednesday, June 25, 2014

Niliolewa na kaka yangu sehemu ya 2

 NILIOLEWA NA KAKA YANGU SEHEMU YA PILI.....

'Mungu chukua uhai wangu..chukua uhai wangu nimechoka kuishi mateso ya dunia'
Baba alimsogelea mama huku mkono wake wa kulia umeshika mkanda wa suruali yake. Mama akiwa uchi wa mnyama, amejikunja chini kwa uoga kama kifaranga. Mama Hamis naye amekaba shingo yangu; kunizuia nisiokoe maisha ya mama yangu. Mdogo wangu Shadrack yupo pembeni ya mama analia kama yatima. Bila huruma, bila kujali baba aliinua mkono wake wenye mkanda na kuanza kumsulubu mama mbele ya macho yetu. Mbele ya hawala yake.
Mama Hamis alishangilia 'kufa wewe kufaaaa mchawi'. Nilipatwa uchungu sana. Huu ni unyama. Siwezi kuyavumilia haya. Nilijitahidi kujitoa katika mikono ya mama Hamis; lakini nilishindwa. Mama aliendelea kupokea vipigo kama punda. Nikakumbuka kuwa mdomoni nina siraha. Meno. Niliyatumia meno yangu na kuuma mikono ya shetani aliyekuwa amekaba shingo yangu bila huruma. Akapiga kelele "huyu mjusi ananiumaa....ananiumaaaa".
Aliniachia na kunipa nafasi. Nilimfuata baba na kumshika miguu yake, nikatumia meno yangu kutafuna mguu wake. Akageukia upande wangu na kunipiga kwa mkanda. Sikujali. Nilikuwa nimepandwa na hasira kama mtu aliyepandisha mapepo. Huku napiga kelele 'nitakuua nitakuua nitakuua' . Machozi yalikuwa yananitiririka kama maji. Baba alijitahidi kunisulubu, lakini sikuachia mguuu wake. Niliyatumia meno yangu ipasavyo. Mama alipoona hivyo; akapiga kelele "Irene..Irene mwache...mwache huyo ni baba yako". Hapana sikuwa tayari kumwacha. Hasira ilikuwa imepanda na kunifanya nionekane kama mbwa kichaa.Mama Hamis alibaki anashangaa. Sikujali. Kelele za mama yangu ambaye yupo uchi, za kutaka nimwachie shetani anayetutesa zilipandisha hasira zaidi.
Nikapiga kelele zaidi huku nalia; kama kichaa 'nitakuua nitakuua...nitakuua'. Kitendo hicho kilimshtua baba. Ilikuwa ni vita kati ya mtoto wa kike wa miaka nane na baba mwenye zaidi ya miaka 35. Nilikuwa nimechoka kuona mama anateswa.  Baba akaona vipigo vya mkanda havitoshi, akaamua kunikaba shingo. Nilijitahidi na kumshika sehemu isiyoshikika. Ni hasira hizo. Mama aliinua mikono yake na kufunika mdomo wake, kama ishara ya kutokuamini anachokiona. Kitendo hicho na hasira zangu zilimfanya baba aogope. Aliniacha na kusogea pembeni. Nilimfuata kwa ujasiri bila kujali huku nikiendelea kusema nakuua nakuua leo.Mate yalikuwa yananitoka kama mbwa kichaa. Baba alinizuia na kusogea pembeni zaidi. Mama Hamis akasema ; " Mmmh Huyu mjusi amekuwa kichaa". Baba hakumsikia. Bado alikuwa anahangaika kunikwepa. Kichaaa kilikuwa kimenipanda. Hali ilikuwa ni mbaya. Nilikuwa nimeamua kufia kwenye mikono ya baba yangu mzazi. Nikasikia mlango wa sebuleni unafunguliwa. Ni jirani yenu Mama Boni.
"Mungu wangu, hii nyumba hamchoki ? Kila siku ni ugomvi tu. Tumewachokaaaa". Mdomo wake ulikuwa wazi; kwani bado hakuamini anachokiona. Mama yupo uchi, na mimi napigana na baba yangu. Ni zaidi ya maajabu.
Mama Hamis akamjibu kwa kupindisha mdomo wake "Hayakuhusu".

Mama Boni, alipatwa na hasira. Akajibu "Wewe mwanamke unatudharirisha. Ndoa yako imekushinda na sasa umeamua kuharibu ndoa za wengine. Hawa wanandoa hawakuwa hivyo, wewe ndiyo chanzo cha yote kutokana na ukahaba wako".
Maneno hayo yalimfanya mama Hamis atukane matusi ya nguoni. Mama Boni hakuyavumilia hayo, alimfuata na kumkaba shingo. Baba alivyoona hivyo, akawasogelea na kumsaidia mama Hamis kwa kumsukuma mama Boni pembeni. Mama Hamis alivyoona hivyo, akatoka nje.Baba alimfuata huku akiita "Darling...please usiondoke".
Mama aliangua kilio zaidi. Mama Boni alikuja na kumfunika kwa kanga yake huku akilalamika "Mama Irene, mbona unateswa sana. Unapigwa ukiwa uchi mbele ya watoto wako? Unyama gani huu jamani?".
Ilikuwa ni aibu ya karne. Mama alilia zaidi kwa huruma. Nilimwonea huruma sana sana. Kilio chake kilitufanya na sisi tulie. Mimi na Shadrack tulimsogelea; na kumkumbatia. Kama watoto yatima; waliotelekezwa. Mama Boni alishindwa kujizuia. Machozi yalianza kumtoka. Akauliza; \
"Mama Irene, achana na hii ndoa".
Mama akajibu kwa kulia ;
"Watoto nitawaacha na nani?"
Mama Boni akasema;
"Ondoka na watoto wako. Katafuteni maisha yenu. Mwanaume mwenyewe alishasema hawa siyo watoto wake. Utamlazimisha? Hebu fanya muondoke. Huyu mwanaume atawaua"
 Mama Boni ni jirani yetu wa karibu sana. Anajua matatizo yetu. Ni jirani pekee ambaye ikitokea tumekosa chakula; ni jirani pekee ambaye huwa anatusaidia. 
Mama akasema ;
"Sina uwezo; ndugu zangu hawawezi kunisamehe kutokana na habari mbaya iliyosambazwa na baba Irene".
Mama Boni akauliza;
"Hivi watu wanavyosema kuhusu watoto wako ni kweli?"
Mama akajibu;
"Hawa ni watoto wake. Sijawahi kutembea na wala kuzaa na kaka yangu. Siyo kweli.Ni uongo uliopikwa na baba Irene"
Maongezi yao yalinishtua kidogo. Sikuelewa nyuma yake kuna ukweli gani.Haya ni maajabu ya dunia. Nilitamani kuuliza; lakini nikaogopa. Ndipo nilipogundua kuwa ndoa ya wazazi wangu imebeba siri iliyo nje ya uwezo wangu. Dunia ina mengi. Ndoa ina mengi; kamwe usitoe maana ya kitu kwa kuangalia nje. Ukweli wa ndani unaweza kukupasua moyo. Maongezi yao yalinipa hamasa ya kujua ukweli zaidi kuhusu matatizo ya ndoa ya wazazi wangu. Nilijua kuwa nikijua ukweli kuhusu ndoa yao; nitajua ukweli kuhusu asili yetu.
                   ITAENDELEA JUMATANO IJAYO...USIKOSE. 
                   TSL BOOKS-Geophrey Tenganamba

No comments:

Post a Comment