Swahili quotes

Friday, June 20, 2014

MAISHA YANGU DUNIANI PART 1: MAHOJIANO KATI YA MUNGU NA MWANADAMU

MAISHA YANGU DUNIANI PART 1: KILA IJUMAA.
Ilikuwa tarehe 12/06/1982, siku nilipokufa na kuondoka duniani. Ni siku niliyokutana na Mungu uso kwa uso, katika ulimwengu mwingine, unaofahamika kwa majina mengi; wengine huita mbinguni, wengine Ahera, kulingana na imani tofauti. Nikiwa nimebeba mizigo yangu ya ndoto nilizoshindwa kuzifikia duniani, mawazo niliyoogopa kuyatoa, vipaji na zawadi nilizopewa na Mungu nivitumie;
Nilipofika geti la mbinguni; nilikutana na malaika. Nilisalimia; kwa heshima. Na kujibiwa;
"Hiyo mizigo ya ndoto zako,vipaji na zawadi za maisha hairuhusiwi  kuingia nayo mbinguni. Mungu alikupa ili itumike duniani na siyo mbinguni. Kwani wewe ulikuwa unafanya nini duniani miaka 89 yote iliyopita? Umekufa ukiwa na miaka 89, hujatumia hata kitu kimoja? Hapana; huwezi kuingia. Ondoka hapa"

Kabla sijapata nafasi japo ya kujieleza, na kutoa sababu ya kwanini nilishindwa kutumia vitu nilivyoumbiwa. Niliwaona watu wawili wanaruhusiwa, ambao ukweli walikuwa na mafanikio makubwa sana sana kipindi walipokuwa duniani. Walikuwa watupu. Hawakuwa na mizigo kabisa. Walikuwa wametumia kila kitu walichopewa na Mungu duniani. Walitembea kwa kujiachia, na kwa maringo. Nilibaki nashangaa, nimesimama kama sanamu; sijui nini nifanye na wapi niende na mizigo yangu. Niliumia sana, sana.
Nilifikiria nilikotoka; Duniani. Mateso ya umaskini niliyoyapitia. Magonjwa na njaa. Manyanyaso na aibu. Nilidhani nikifika huku; nitapumzishwa kama nilivyofundishwa. Niliumia sana; na hapo ndipo nilipojisemea moyoni kuwa lazima, lazima nionane na Mungu mwenyewe. Lazima nipate nafasi ya kumuuliza maswali; aniambie kwanini mimi? Kwanini niliteseka nilikotoka; na huku nilikofika sijayakuta niliyoyatarajia? Nilishangaa sana kuyakuta niliyoyakuta. Nilisogea pembeni kuwapisha wengine. Iliniuma sana. Hii kitu gani tena? Nilitembea pembeni ya geti; kidogo nikaona shimo lefu sana lenye ngazi. Hii kitu gani?
Nikatembea mbele kidogo; nikakuta njia moja ndefu; isiyo na mwisho. Kuna mambo yakaanza kunitokea; kwa lugha ya kidunia ni vigumu kuyaeleza. Nilishangaa sana. Mbona haya mambo sikufundishwa? Yote niliyoyaona, mbingu,kuzimu si kama nilivyotarajia. Nikagundua kuwa mengi niliyofundishwa, mengi niliyoaminishwa yalikuwa ni ya msukumo na mfano wa kidunia na mfano wa mwanadamu na si mfano wa Mungu. Na hata Mungu, mwenyewe niliyeaminishwa ni Mungu wa mfano kwa mwanadamu na si mwanadamu kwa mfano wa Mungu. Hii kitu gani tena?
Nilipokuwa duniani nilifundishwa Mengi; nikaaminishwa mengi nikidhani ni kweli kumbe ilikuwa ni upupu. Nilitamba kwa watu enzi za uhai wangu, nikijiona najua. Nilishika maneno ya vitabu vya dini;niliyofundishwa kama mwanafunzi anayejiandaa kufanya mtihani baadaye; lakini sikuyaishi wala kuyajaribu ili nijue kama ni ya kweli au porojo. Zaidi niliyatumia kuwatenga na hata kuwaua wengine.  Nikachezea miaka 89 ya maisha yangu, bila maana, bila sababu na bila malengo.
Ilipofika tarehe 12/06/1982; nikaondoka bila kuacha kitu chochote cha maana kwa wanadamu wengine duniani.Nimefika huku niliko; nikakuta yale niliyoaminishwa siyo. Lugha inayotumika si lugha ya maneno kama duniani. Nikagundua kuwa kama ningefundishwa lugha hii nikiwa duniani; nisingeishi maisha niliyoishi. Nilidanganywa. Ninajuta. Ninajuta. Niliwauliza malaika kama upo uwezekano wa mimi kurudi tena duniani nikaishi upya. Nikaambiwa nimechelewa. Siwezi kurudi tena. Maisha niliyopoteza; nilipewa mara moja tu na siwezi kupewa tena.
Nikauliza ; hii mizigo yangu inayonitesa niipeleke wapi? sikupata jibu. Nikatamani kurudi japo nikaishi hata kwa siku moja ili nikayaache hata mawazo yangu; lakini siwezi. Nilifanya kila ninachoweza kufanya ili nirudi duniani; haikuwezekana. Na mwisho nikaruhusiwa kuandika barua kwa wanadamu wote; kwa njia ya ndoto kupitia mwandishi iitwayo MAISHA YANGU DUNIANI.
FUATILIA KISA HIKI CHENYE UKWELI WA AJABU KILA IJUMAA. SOMA KITABU HIKI UKIWA UMETULIA; KIMEBEBA UJUMBE UNAOWEZA KUTIKISA IMANI HABA.
TSL BOOKS TANZANIA. Geophrey Tenganamba


No comments:

Post a Comment