Swahili quotes

Tuesday, June 17, 2014

Nikumbuke Mpenzi wangu:Remember me my love Part 1






“Dokta Adam….Dokta Adam hatutaweza kumrudisha mgonjwa  huyu. Lazima tutampoteza”
Ilikuwa ni sauti ya mwanamke niliyoisikia kwa mbali. Nilijaribu kufanya  kila ninachoweza lakini mwili wangu haukuwa na uwezo tena.  Sikujua nipo wapi na kwanini. Macho yangu hayakuwa na uwezo wa kuona. Pua yangu; haikuweza kuambulia harufu yoyote.

Nilianza kujiuliza kuhusu  sauti  ya mwanamke iliyosikika kupitia masikio yangu ikisema Dokta Adam hatutaweza kumrudisha mgonjwa huyu. Lazima tutampoteza. Nilijiuliza mgonjwa huyo ni nani? Je ni mimi au ni mtu mwingine? Na hapa nipo wapi? Nimefikaje?Wakati bado najiuliza maswali yasiyo na majibu nikasikia sauti ya kiume ikisema:
“Patricia..Patricia huwezi kufia katika mikono yangu. Mateso uliyoyapata kwasasa yanatosha. Huwezi kufa. Huwezi kufia ndani ya chumba changu cha operesheni. Huwezi kufa… amka….amka Patricia”
Ilikuwa ni sauti nzito sana iliyobeba uchungu ndani. Nikashtuka ..kwanini Daktari anataja jina langu? Na hapa hospitali nimefikaje? Na Daktari huyo ni nani? Amejuaje jina langu? Mume wangu mpenzi yuko wapi? Wanangu wako wapi? Wazazi wangu wako wapi?Mwili wangu haukuwa na maumivu kabisa. Hiyo ilinishangaza zaidi. Macho yangu hayakuwa na uwezo wa kuona kabisa. Kwangu ilikuwa ni giza nzito. Kila nilipojaribu kufumbua macho yangu japo niwaone watu walio pembeni yangu; nilishindwa. Kope za macho yangu zilikuwa nzito zaidi ya gunia la mchanga. Ni kitu gani kinaendelea? Nimetokewa na nini mimi?
Nikasikia sauti ya mwanamke kwa mara nyingine ….”Dokta Adam..Dokta Adam bado siwezi kurudisha mapigo yake… yupo mbali sana.  Pia katika kifua chake vidonda ni vingi mno. Anatoa damu sana kama bomba la maji. Siwezi kufungua kifua chake, amefungwa bandeji nyingi sana. Hakuna nafasi Dokta…Inaonyesha amepoteza damu nyingi sana kabla ya kuokotwa msituni alikotupwa na kuletwa hapa. Huyu mgonjwa hatutawezia kumrudisha… hatuwezi”
Niliposikia sauti hiyo niliogopa zaidi. Nilizidi kujiuliza; nimetokewa na nini  mimi? Daktari alitoa sauti ya ukali :
“Dokta Anna..hivi wewe ni daktari au afisa masoko? Mbona unapiga kelele ambazo hazina msaada kwa mgonjwa? Fanya ninavyokuelekeza. Acha kuongea ongea kama mwanasiasa. Hii siyo siasa; hapa tunahitaji kurudisha uhai wa mtu na siyo kupiga makelele. Mgonjwa akipona au akifa ni biashara yangu na siyo yako. Kama huwezi mlango upo wazi, toka na umwite Daktari msaidizi mwingine”
Sauti ya Daktari ilinifanya niamini kuwa Daktari hataki kuniruhusu niondoke mapema nikakutane na muumbaji wa mwili wangu. Na ni mwanaume wa kwanza kujali uhai wangu. Kama Mungu amepanga  nifie ndani ya chumba hiki bila kujua nimefikaje; sina pingamizi. Mume wangu yuko wapi? Wanangu wapenzi Angelina na Abeli wako wapi?.
Sikujua ni kitu gani kitatokea baada ya hapo. Sikujua kama nimekufa au nipo hai. Nikiwa sijui ni kitu gani kinaendelea, nikasikia sauti ya mashine iliyokuwa imeunganishwa na moyo wangu. Sauti ilikuwa kubwa yenye mlio wa honi ya gari…biiiiiiipu……………………biiipu……biiipu….biiipu. Nikakumbuka filamu kadhaa za hospitali nilizowahi kuziona. Jinsi inavyotokea watu wanakufa. Nikagundua kuwa na mimi naelekea huko. Na hata madaktari waliokuwa wananihudumia; walianza kuchanganyikiwa. Ilikuwa ni siku yangu. Imefika mimi kuondoka kwenda kuonana na Muumbaji wa dunia. Nikaanza kusikia utulivu ndani yangu, hiyo ilinishtua zaidi. Kilichonishangaza; sikuwa na uoga kabisa wa kufa. Kitu cha ajabu  ni kwamba bado nilikuwa palepale. Ndani ya mwili wangu nimetulia tuli. Nilitakiwa kutoka ndani ya mwili wangu; lakini bado nilikuwa nimeshikwa na kufungwa mwilini. Gizani. Sioni mwanga mweupe wala chochote wala mtu yeyote wa kunipokea na kunionyesha mbinguni; au hata malaika wa kunielekeza. Nilikuwa nimekwama mwilini kama mtu aliyetupwa ndani ya shimo lenye giza na hawezi kutoka. Sikuwa na uwezo wa kuona chochote zaidi ya sauti ya madaktari na vyombo vyao wakihangaika kurudisha uhai yangu.
Nikasikia sauti ya Daktari ikisema “ Nipe Difibrileta…Difibrileta…badilisha pandisha mpaka ishirini. Piga kwa atropine.  Michael njoo haraka unisaidie. Mgonjwa huyu hawezi kufa….hawezi kufa…no …no”
Dokta Adam tayari alikuwa ameshachanganyikiwa.  Alijua sekunde kadhaa zijazo nitakuwa nimeondoka kwenda kupumzisha ubinadamu wangu.  Alitoa amri kama mwanajeshi. Na wote walifanya kulingana na maelekezo. Tena kwa haraka. Nikasikia sauti ya Dokta Adam…
“Clear”……kisha nikapigwa na kifaa kifuani kama shoti ya umeme na mwili wangu ukarushwa juu. Sikujua ni kitu gani. Labda walikuwa wanajaribu kunirudisha kutoka wafu.  Ilinipa shida sana kwani sikuweza kuona wala kuhisi chochote katika mwili wangu. Nilitamani kuona kinachoendelea lakini sikuweza. Nilikuwa gizani. Giza la peke yangu. Mbingu haikuwa nami na dunia ilikuwa imenitelekeza. Nilifikiria jinsi nilivyo. Mwili wangu umekuaje?
Sikuwa na kumbukumbu ya yote yaliyotokea siku hiyo wala yaliyotokea wiki iliyopita. Nilichokumbuka ni kuwa mimi ni mke wa Mr. Osward Tesha. Na nina watoto wawili, Angelina na Abel.  Baada ya dakika kadhaa nikasikia sauti ya mashine inalia kwa nguvu. Dokta Adam akalalamika kwa sauti.
“No…No… usife…lazima upone ili ujue unyama uliotendewa na mtu wa karibu yako”.
Nikashtuka; unyama niliotendewa? Kivipi? Na kwanini?  Dokta alipumua kwa nguvu sana na kusema “ Michael pandisha hadi mia themanini. Sintakubali kumpoteza dada huyu sintakubali. Debora naomba iongezwe damu AB-negative. Na maji zaidi haraka sana”
Sauti ikasikika tena:
“clear”. Kisha mwili wangu ukarushwa  juu na kurudi tena katika ile meza ya operesheni. Na kwa sauti ya chini mashine ikalia  biiiiiiiipu….biiiipu. 
ITAENDELEA SIKU YA JUMANNE. USIKOSE

TSL Books-by Geophrey Tenganamba

No comments:

Post a Comment