Swahili quotes

Tuesday, June 24, 2014

Nikumbuke Mpenzi wangu part 2

Mungu nimekosa nini. Mungu nisaidie.....Nikasikia sauti ya madaktari wakipumua kwa furaha. Michael akasema; "Dokta...umemrudisha". Wote kwa pamoja wakafurahi. Dokta Adam alionyesha kufurahi zaidi. Sauti yake ya furaha; ilipenya ndani ya masikio yangu. Hii ilinipa amani; nikajua labda nimerudi. Wote wakavua glovu na kuzitupia ndani ya chombo cha kuutupia uchafu. Niliwasikia kwa makini sana, nilitaka kujua ni kitu gani kinaendelea. Baada ya dakika kadhaa nikasikia sauti ya Debora.

"Dokta, nimekuja na damu na vifaa ulivyoniagiza. Ah mgonjwa amerudi? Mungu mkubwa".
"Okay hakikisheni ameshonwa vizuri. Mpakeni antibiotiki, mtundikieni damu na mfanye kwa uangalifu sana. Hakikisheni hamtoki humu ndani. Tena inabidi mhudumu mwingine aongezeke. Huyu mgonjwa anahitaji ulinzi mkali sana. Hatakiwi kubaki peke yake hata kidogo. Maisha yake yapo hatarini zaidi ya hali yake. Mimi ninaenda polisi kuripoti kesi yake. Nitarudi baadaye kwaajili ya uangalizi zaidi"
Maneno ya Dokta Adam yalinipa shida sana. Nipo hatarini? Kwanini? Ni kitu gani kimetokea katika maisha yangu? Nimefanya kosa gani duniani?Na kwanini daktari anaenda polisi? Mume wangu yupo wapi? Bado kichwa changu kimejaa maswali yasiyo na majibu; na sina uwezo wa kuuliza japo kupata majibu hayo. Sauti ya mlango ilisikika ukifunguliwa na kufungwa. Dokta Adam alikuwa anaondoka. Kuondoka kwa Dokta Adam nilijisikia mpweke sana. Nimeachwa mimi. Sikujua kwanini, labda kwasababu ni mwanaume pekee aliyeonyesha kujali sana kurudisha uhai wangu. Madaktari na wahudumu waliobaki; walionyesha kama wamemaliza kazi na sasa wanasubiri mimi niamke. Ingawa sikuona tofauti yoyote wala maendeleo. Hiyo ilinipa shida. Bado sikuwa na uwezo wa kunusa, kuona, kutikisika. Mwili wangu ulikuwa hauna mawasiliano na mimi. Lakini kwasababu ya furaha ya madaktari, nikahisi labda nimerudi kutoka wafu lakini bado nipo mahututi.
Baada ya dakika kadhaa nikasikia mashine, ya kusaidia kupumua kwangu inalia. Wahudumu wakaanza kuhangaika tena.
"Oh..no anapotea tena. Tunampoteza jamani. Mwiteni Dokta Adam..mwiteni dokta Adam haraka sana"
Ilikuwa ni sauti ya Michael. Mlango ulifunguliwa na sauti ya mwanamke, Debora alisikika akiita "Dokta Adam....Dokta Adam....mgonjwa mgonjwa ...mgonjwa"
Michael alikuwa anahangaika na wahudumu waliobaki. Wote wanalalamika. Walionyesha kukata tamaa. Mimi sikujua ni kitu gani tena kimebadilika; labda nilikuwa naondoka kwenda kwa Mungu. Furaha yote waliyokuwa nayo ilipotea. Sikujua kama nipo mahututi au nimekufa. Kila kitu kwangu ilikuwa ni sawa tu. Japo nilikuwa na maswali ya kutaka kujua ni kitu gani kimenitokea katika maisha yangu. Sikuwa na uoga wa kifo; wala shauku ya kurudi. Labda kwasababu sikujua kama nimekufa. Nikasikia sauti ya mlango ukifunguliwa. Alikuwa ni Dokta Adam.
"Nini tena kimetokea?" Sauti yake ilipenya moyoni mwangu, nikasikia amani ya moyo. Jambo moja nina uhakika; alipoingia Dokta Adam tu upweke wote ulipotea kama upepo. Sikujua ni kwanini. Na baada ya hapo mashine, ikaacha kulia kama mwanzo. Na madaktari wote wakashangaa.
"Dokta Adam, mimi sielewi. Yaani baada ya wewe kuingia mgonjwa amerudi. Ulipoondoka dakika mbili zilizopita mapigo yake yalianza kupotea. Dokta au wewe ni Mungu?" Michael alisema.

Dokta akaguna ahh...Mimi sikujua kwanini hali yangu imebadilika baada ya Dokta Adam kurudi. Michael akaendelea ;
"Dokta, una nguvu za kimungu. Hii siyo kawaida"
Dokta akajibu "Wewe acha kufuru. Mungu ni mmoja tu. Mimi siyo Mungu na wala unayosema siyo kweli; ni hali ya kubahatisha tu. Jamani mimi sijalala kabisa leo; pia nahitaji kurudi nyumbani nikasalimie familia yangu. Nina siku mbili hapa hospitali sijarudi nyumbani. Pia nahitaji kwenda polisi kwaajili ya kesi ya huyu dada. Tafadhali mwangalieni; mimi ni lazima nitoke muda huu ...please guys"

Sikujua kwanini uwepo wa Dokta unanifanya nijisikie vizuri. Nilihitaji uwepo wake. Nilitamani asiondoke.
Dokta Adam akaendelea ;
"Sasa ndugu zangu , huyu dada kama nilivyowaeleza mwanzoni anahitaji ulinzi sana. Na watu wa kuogopwa, tena hawaruhusiwi kabisa hapa hospitali ni ndugu zake na watu wa karibu yake"
Kwanini ndugu zangu hawaruhusiwi? Ni hatari kwangu? Mume wangu je? Watoto wangu je? Na wazazi wangu je? Wote hawaruhusiwi? Nilihisi masikio yangu yamesikia kitu ambacho sicho. Michael akauliza;
"Kwanini ? Unataka kusema ni ndugu zake na watu wa karibu wamehusika?

Dokta akajibu "Hupaswi kujua kwa undani. Ni hatari kwako zaidi ya unavyofikiria. Kumbuka kuwa anayeweza kukudhuru na kukuumiza zaidi ni yule aliye karibu yako. Mpenzi wako. Wazazi wako. Ndugu zako. Kuwa mwangalifu. Dunia ni kama jangwa lenye takataka"

ITAENDELEA JUMANNE IJAYO;
                    TSL Books-geophrey tenganamba

No comments:

Post a Comment