Swahili quotes

Wednesday, June 18, 2014

NILIOLEWA NA KAKA YANGU: I married my blood brother part 1.



NILIOLEWA NA KAKA YANGU: Based on a true story KILA JUMATANO. 
Nikasikia sauti kutoka moyoni  mwangu ikiniambia “Tulia moyo wangu. Tulia mwanangu haya yote yatapita. Haya yote yataisha. Ipo siku, ipo siku dunia yako itabadilika”.
Niliposikia sauti hiyo nilifuta machozi na kukificha kisu, ambacho kama siyo sauti hiyo ningemchoma baba yangu mzazi tumboni. Nilikaaa chini kuyasikilizia maumivu.  Baba yangu hakuonyesha kujali; aliendelea kumpiga mateke mama yangu. Nilishindwa kuyavumilia, ndiyo nilishindwa kuyavumilia nilimsogelea na kumchoma mapaja yake.Kwasababu sikutumia nguvu kutokana na uoga; sikumuumiza. Alinigeukia na kunikanyaga bila huruma bila kujali kuwa mimi ni mtoto wa miaka nane. Mama akapiga kelele; 


“Kama umepanga kuniua , niue mimi na siyo wanangu. Hawana makosa, na wala hawakuchagua kuzaliwa kupitia sisi”.  

Mdogo wangu Shadrack  mwenye miaka mitano alikuwa analia kwa uchungu sana. Wazazi wangu hawakujali, waliendelea na vita vyao. Nilianza kujuta kuzaliwa; katika familia yangu. Nilitamani kuzaliwa upya, katika familia nyingine. Baba yangu alirudi upande wa mama yangu; akachukua chakula tulichopika na kumwaga bila kujali kuwa toka asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni hatujatia kitu mdomoni. Haya ni maisha gani? Haya ni mateso gani? Tumemkosea nini Mungu  sisi? Mama alilia kwa uchungu kwa kupiga kelele sana;
“Baba Irene, usiniue. Usiniue”.
 Baba hakujali, alimpiga makofi ya usoni, mateke na kumtukana matusi ya nguoni mbele yetu. Siwezi kuyasema matusi hayo hapa. Yanatisha sana. Baada ya hapo; akatoka nje huku bado anatukana. Na kuondoka zake.  Kilichonishangaza hakuna hata jirani yeyote wa karibu aliyekuja kuamua ugomvi wa wazazi wetu. Labda kwasababu katika mtaa wetu ilikuwa imezoeleka. Kila mtu alikuwa anajua kuhusu familia yetu.  Nilijiuliza mengi sana kuhusu familia yetu, vita ilikuwa ni jadi yetu. Sikuona umuhimu wa familia. Zaidi niliwachukia wanaume sana. Kila mwanaume nilimuona kama aina fulani ya shetani asiyestahili kuishi.
Baada ya baba kuondoka; mimi na Shadrack tulianza kuokota viazi vilivyomwagwa na baba. Tulivyopika; kama chakula cha mlo mmoja. Mama hakuwa na nguvu. Aliendelea kulia; kama mtoto mdogo aliyetelekezwa na ndugu zake.  Maisha hayakuwa upande wetu. Mama akajitahidi kuinuka; akasema “Irene, viosheni hivyo viazi. Kuleni, mimi naenda kulala”.
Nikamwambia  “Jitahidi mama, ule hata kidogo”.
Aliniangalia kwa huruma na kuondoka kwa kujikongoja.Nilimsindikiza kwa macho na kuanza kumwangalia mdogo wangu Shadrack, bado ni mtoto. Hana nguvu wala afya. Baadaye yake, baadaye yetu itakuaje? Niliogopa sana. Nikaanza kulia; akaniambia “Dada Ina Dada tulia..tulia…asilie Dada ina”. Alinitia uchungu sana. Nikiwa na miaka nane, tayari akili inaamini kuwa  dunia si mahali bora kuishi. Ni kuzimu iliyotengenezwa na Mungu.  Dunia yetu ilikuwa ya upweke. Isiyo na chochote zaidi ya mateso na machozi.
Tulikula viazi na kunywa maji. Tulipomaliza nilimwacha mdogo wangu anacheza jikoni. Nikachukua viazi na maji na kumfuata mama chumbani. Nilikuta bado mama analia kwa uchungu. Nikamsihi asilie; “Mama usilie…Mama usilie”. Moyo wangu ulijawa hasira, hasira kali ya kuua. Nilipanga kutafuta njia ya kumuua baba yangu. Mama yangu akadakia kana kwamba amesikia mawazo yangu;
“Mwanangu Irene. Kamwe usije mfanyia baba yako ubaya wowote. Mimi pia nina makosa niliyomkosea. Natamani kuondoka duniani, lakini wasiwasi wangu ni nyie. Mtaishije peke yenu katika dunia hii isiyo na huruma?”
Nilimwangalia kwa kumshangaa. Nilijiuliza; iweje mtu akutese na kukufanyia unyama kama huo lakini bado uendelee kumsamehe na kuishi naye? Watu wanasema ndoa; ndoa kitu gani? Mungu hakutengeneza ndoa kwaajili ya mateso. Mungu hakutuleta duniani kuteseka; sintakubali. Sintakuja kuolewa. Nilikaa na mama mle chumbani, mpaka ilipofika saa moja na nusu jioni. Nilirudi jikoni na kukuta Shadrack amelala; nilimbeba na kumpeleka chumbani kwetu. Uchungu ulinijaa moyoni. Sikuona utamu wa maisha duniani. Wala sababu ya kuishi duniani. Kila kitu kwangu. Mawazo yangu; yote ilikuwa ni kulipiza kisasi. Kuwatenda wanaume. Hata ikibidi kuua; kama nikipata nafasi kipindi cha ukubwa wangu.
Nilijikuta nimelala; mpaka nilipokuja kushtuliwa na kelele za wazazi wangu tena. Nilisikia kelele za watu watatu. Baba, Mama na mwanamke ambaye; ni mke wa pili kwa baba; mama Hamis. Ni mama ambaye; alikuwa ni mke wa mtu akaachika kwasababu ya mahusiano yake yeye na baba. Nilitoka sebuleni; Shadrack alinifuata nyuma. Ilikuwa ni saa nne usiku. Tulipofika sebuleni, tulikuta mama Hamis anacheka. Alipotuona; akasema "Nyie mijusi rudini chumbani mkalale. Haya mambo hayawahusu".
Nilitamani nimshike, nimfinyange,nimtafune na kumzika. Mwili wake ulikuwa mkubwa; alikuwa ni aina ya mtu anayekua kwa kutanuka. Mnene kama nguruwe. Mama na baba walikuwa chumbani. Nilisikia vipigo vya mateke; mama alikuwa anapiga kelele. "Ananiua...ananiua...ananiua". Nilipojaribu kukimbia kwenda chumbani kumsaidia mama. Nilikabwa shingo na mama Hamis, nikaanza kupiga kelele.."Niache shetani..niache shetani". Mdogo wangu Shadrack alianza kupiga kelele. Ghafla..mama alisukumwa mpaka sebuleni kutoka chumbani, akiwa uchi. Uchi wa mnyama. Nililia. Nililia. Na kulia. Nikajitahidi kufumba macho, japo nisiyashuhudie ninayoyaona. Mdogo wangu Shadrack alimkimbilia; na kuanza kulia pembeni yake. Mama Hamis alicheka sana. Baba alitoka nje kwa spidi; huku ameshika mkanda wake wa suruali. Nililia zaidi na kusema Eee Mungu uko wapi? Naomba uchukue uhai wetu. Tumechoka kuishi katika dunia uliyotuleta. Mungu....Mungu...

ITAENDELEA JUMATANO IJAYO. 
TSL BOOKS-Geophrey TENGANAMBA
 
 

No comments:

Post a Comment