Swahili quotes

Sunday, June 29, 2014

Naijutia Ndoa Yangu Sehemu ya pili

Mama yangu mzazi Eugenia Mwafilombe na baba yangu wa kambo Patrick Sichalwe hawakutoa kitu. Hata zawadi ya pipi; iliniuma sana. Lakini nilimshukuru Mungu kuwa siku ya harusi walifunga midomo yao; hawakutoa siri ya yote niliyofanya ili niolewe na Benson. 

Baada ya hapo zilianza kutajwa zawadi za nyumba kubwa mbili Msasani peninsula; na nyingine Mbezi beach. Na gari mbili kwaajili ya Benson. Mashamba na viwanja pamoja na kampuni ya East Insurance Ltd kama zawadi zetu za kuanzia maisha yetu.
Hamu ya kuanza kutafuna utajiri ilianza kuniingia kama mbwa anavyotamani mnofu wa nyama ya ng'ombe. Nilifurahi sana kwani nilijua maisha yangu ndani ya ndoa yatakuwa kuku kwa mrija. Nilianza kupiga hesabu za  kusafiri nje kustarehe na honey moon yetu iliyopangwa ifanyike South Afrika. Kila kitu  siku hiyo kilionekana kama maandalizi ya raha zaidi mbele yangu.

Baada ya muda wa zawadi; Mhe. Rais pamoja na wageni wakubwa Serikalini walisimama na kuondoka. Wageni waalikwa waliruhusiwa kutoa zawadi; na kuanza kuselebuka kwa muziki. Baada ya saa moja; MC aliturhusu tuondoke ili tukajiandae kwaajili ya safari yetu ya South Afrika. Tuliondoka huku tukishangiliwa kama washindi fulani tulioshinda tuzo.
Tulitoka nje ya ukumbi tukapokelewa kama wafalme wa Uingereza na kuongozwa mpaka kwenye gari letu lililokuwa limepambwa na kung'aa kama dhahabu. Msafara wetu wa kwenda Oysterbay nyumbani kwa Ben ulianza. Ilikuwa imefika saa sita usiku. Nikamuomba Benson tuahirishe safari yetu usiku huo na tuondoke kesho yake asubuhi au mchana ili tupumzike kwanza; alikataa katakata na kunibembeleza sana tuondoke usiku huo.
Ndege yetu ilipangwa kuondoka saa nane usiku; ukweli sikujua ulazima kwa kusafiri usiku huo. Niliamua kukubali kwa shingo upande. Nilikuwa naogopa kwani ni mara yangu ya kwanza kupanda ndege. Na zaidi itakuwa ni usiku. Benson alinitia moyo kwa kunibusu.
"Usijali Jack wangu. Tutapumzika ndani ya ndege. Imeandaliwa maalumu kwaajili yetu. Na kwaajili ya starehe zetu".
Nilipata imani kutokana na maneno yake. Tulifika nyumbani kwa Ben saa sita na nusu.Na kupokelewa na wifi zangu waliokuwa wanatusubiri kwa hamu. Tulipoingia nyumbani kwa Benson kwa mara ya kwanza; nilihisi nipo peponi. Nyumba yake ilikuwa ni ghorofa ya juu; wazungu wanaita Apartment; yenye vyumba vinne.
Chumba chake; kilikuwa kinaangalia upande wa bahari wazungu wanaita sea view. Kikubwa zaidi au mara tatu ya nyumba yetu ya urithi iliyojengwa na marehemu baba yangu; ambaye mpaka leo sijui sababu ya kifo chake. Ben alinishika mkono na kunisogeza kitandani. Nilisogea kwa uoga kutokana na ugeni wa yote ninayoyashuhudia. Akaniuliza "Mbona unashangaa kana kwamba ni mara yako ya kwanza kuingia ndani ya chumba hiki?"
Hakujua ukweli. Hakujua; mimi siyo Jackline anayemjua. Nikajibu ; "Hapana nimefurahi tu"
Akauliza tena "Jack Mbona ulivyokuwa mwanzo si sawa na ulivyo sasa?"
Nikaogopa; nikidhani labda siri yangu imeshajulikana. Niliwaza sana kabla ya kujibu kwani ukweli wa yote ninaujua mimi na mama yangu. Ni siri kubwa ya kafara ya rafiki yangu Jackline niliyoifanya ili nichukue nafasi yake. Ukweli kwa jina ninaitwa Emelda John; lakini sura yangu ni ya Jackline Stephano. Kuna mengi nitakujuza; endelea kunifuatilia. Siri hii ni siri yangu na mama yangu; na nipo tayari kutoa hata uhai wa mama yangu pia kama ikitokea anahatarisha ndoa yangu.
Sintaruhusu mtu yeyote aijue mpaka nitakapoingia kaburini. Benson anadhani aliyeoa ni Jackline Stephano; nitahakikisha yeye pamoja na ndugu zake wanaishi na kuamini hivyo ili ndoa yangu idumu na kudumu. Mungu anisamehe kwa yote na aniache niishi ndani ya ndoa hii kwa furaha. Benson akanishika mkono na kuuliza;
"Jack unakumbuka meno yako mawili ya mbele yalikuwa yameoza; mbona siku ya leo meno yako ni meupe pee. Umefanyaje?"
Swali la Ben lilinipa wasiwasi; nikaanza kuhisi kuwa labda Ben amejua siri. Hapana. . Nikajipa moyo; vyovyote itakavyokuwa iwe. Ndoa hii ni yangu. Utajiri huu ni wangu. Na Benson ni mume wangu. Nilimwangalia usoni kwa kutumia uzuri na nguvu ya macho yangu kulingana na maelekezo niliyopewa siku ya kafara. Na nikajisemea moyoni;
'Mimi ni nguvu. Mimi ni mwanamke wa nguvu mwenye mamlaka makubwa ya kuharibu au kutengeneza; kulaani au kubariki. Kwa uwezo wa sumaku iliyo ndani ya macho yangu. Na nguvu ndani yangu; mwanaume huyu pamoja na familia yake wapo chini ya himaya yangu. Chini ya utawala wangu. Nitakachokisema kiaminike, kikubalike na kitekelezeke'.

Baada ya maneno hayo nilimbusu na kumjibu.
"Haya meno ni ya bandia. Daktari aliniwekea na akasema nina bahati kwasababu meno yangu yameendana na mfumo wangu. Hivyo yatadumu na kuonekana kama meno ya kweli"
Benson alitabasamu na kunifurahia; kisha akasema;
"Tuoge na kujiandaa ili tuanze safari; muda unaenda"
Kwa pamoja kama mapacha; tulibadili nguo zetu na kuanza kucheza kama mapacha. Na kuingia ndani ya jakuzi lenye maji ya moto; tulioga huku tukifanya ya kwetu na kupeana raha na mikwara jinsi itakavyokuwa huko South Afrika kwenye honey moon yetu. Benson alikuwa mwanaume wa pekee sana. Ninashukuru Mungu kuwa kwasasa yupo chini ya himaya yangu. Ninaomba ndoa yetu idumu mpaka siku ya vifo vyetu.

ITAENDELEA JUMATATU IJAYO.....
TSL Books-geophrey tenganamba

No comments:

Post a Comment