Jinsi ya
Kuthibiti Hasira
Maisha ya mwanadamu ni mzunguko wa changamoto mbalimbali, kila dakika ya maisha yako, kila sehemu uliyopo na kila mahusiano uliyonayo vyote vimebeba changamoto na maana Fulani ya maisha yako.
Wote tunapitia maumivu,machungu, makwazo , kero na mifumo ya aina moja lakini kinachomtengeneza na kumboresha mtu si yale anayoyapitia - bali ni yale anayoyafanya kutokana na yale anayoyapitia. Katika mahusiano tunakumbana na watu,marafiki na hata wapenzi wetu wanaotupandisha hasira na mara nyiningine wanaotutenda vibaya haswa, lakini cha muhimu kufahamu ni kuwa yote haya ni shule ili tukue na tupanuke zaidi.
Kila binadamu ana mategemeo Fulani katika mahusiano aliyonayo na watu wake wa karibu. Wote tunaishi katika dunia yenye majaribu, tunazungukwa na watu ambao si wote wanatambua nini tunatarajia kutoka kwao. Kutokana na hayo hatuwezi kuepuka kukasirishwa lakini tunaweza kuepuka madhara ya hasira kwa kuthibiti hasira zetu kutokana na mahusiano yetu.
Hasira ni hali ambayo haiwezi kuepukika katika mahusiano lakini inawezekana kabisa kuthibitiwa.
Hasira ni hisia, ni uchaguzi kama ilivyo katika tabia. Inaweza kuthibitiwa, na inaweza kutumiwa kimanufaa. Kuwa na hasira, si dhambi na wala si kosa lakini yale unayoyafanya kutokana na hasira ni kosa na ni dhambi na mara nyiningine pia huwa ni kinyume cha sheria. Hasira ni hisia ya kiasili ndani yetu,ni hisia ya ulinzi na utetezi ili kutufanya tukue na si kwa ajili ya kushambuliana. Hasira si kubeba kinyongo katika maisha bali ni kutafuta maana. Hasira si nguvu kwaajili kuumiza mtu bali ni nguvu kwa ajili ya kukusaidia wewe kutafuta hatua ya nguvu yenye kukufaidisha.Ni kweli na dhahiri kuwa hasira inaweza kuharibu,kuvunja ndoa,mahusiano na hata kusababisha mashambulio kama isipothibitiwa kwani, vita vyote vinavyotokea duniani, mauaji na hata chuki vyote ni matokeo ya hasira. Binadamu ni wa maana, tuna uzuri ndani yetu hata kama ni kweli hutujakamilika kutokana na mapungufu Fulani , lakini tunao uwezo wa kuthibiti hasira zetu, na kuzitumia kimanufaa. Ikumbukwe kuwa hasira isiyothibitiwa hutengeneza majanga.Na mwanadamu mwenye hasira ndiye anayedhurika zaidi. Kuwa na hasira au kubeba kinyongo ni sawa na kubeba makaa ya mawe yenye moto kifuani kwa nia ya kumtupia mwingine, lakini anayeumia na kuungua ni wewe zaidi. Hasira ni wazimu kwa kifupi, kwani yeyote anayefanya jambo kwa hasira hutumia sana mwili kuliko akili. Hasira ni sumu inayoondoa uzuri wa ndani, ni mmemenyuko wa uzuri wa binadamu. Hasira lazima ithibitiwe. Mwanadamu asiyethibiti hasira hana tofauti na mwendawazimu. Jambo lolote linaloanza na hasira lazima liishie na janga.Kila dakika unayokuwa na hasira unapoteza sekunde sitini za furaha na maisha yako. Hasira hasara!Ni muhimu kuithibiti hasira kwa kutambua kuwa; katika maisha unao uchaguzi wa kukasirika au kutokasirika. Unao uhuru wa kuweka kinyongo au kuamua kumuelewa, kumsamehe na hata kumpotezea aliyekukasirisha. Katika hasira zako unao uhuru wa kulipiza kisasi au kujifunza kutokana na yale uliyoyapitia na kuwa na kinyume na makosa uliyotendewa. Kila kitu duniani kinachotokana na hisia zilizondani yako, unao uhuru wa kuchagua na kuthibiti. Kumbuka kuwa maisha yako si kutokana na yale unayotendewa bali ni kutokana na yale unayochagua kuyafanya kutokana na yale unayotendewa.Hasira ni uchaguzi, hasira ni maamuzi. Ikumbukwe kuwa hasira ya muda mrefu haikai katika vifua vya watu wenye busara, lakini hubakia vifuani mwa wapumbavu. Na yeyote anayekufanya ukasirike na ukakubali kukasirika hushinda dhidi yako.
P.o.box 78805Thibiti hasira yako kwa kutambua yafuatayo;
- Tambua kuwa wewe ni binadamu mwenye uzuri ndani yako, uliye zaidi ya hasira na mwenye uwezo wa kuthibiti hasira yako
- Tambua kuwa katika kila mahusiano, wewe ndiye mwenye uhuru wa kuchukia ama kufurahi.
- Wewe ni bustani ya maisha, furaha na mazuri yote ya dunia. Furaha ya maisha yako si kutokana na watu na hali za nje yako bali ni kutokana na yale ya ndani yako
- Tambua kuwa mahusiano mazuri ni yale uliyoyajenga ndani yako mwenyewe na si kutokana na watu wanaokuzunguka. Tengeneza mahusiano mazuri na wewe mwenyew
- Unaweza kuthibiti hasira yako kwa kuamini kuwa wewe ndiye unayetengeneza hasira na hata kuiharibu/kuikataa hasira
- Tambua kuwa kama ilivyo kweli kuwa una mapungufu yako, hali kadhalika hata wanaokuzunguka wana mapungufu yao. Thibiti hasira kwa kuishi katika uelewa huo.
Rafiki yangu - Maisha ni shule, ni mapito na ni mitihani , binadamu watakaoweza kujifunza na kukua zaidi ni wale wanaoishi kwa kuamini kuwa mazuri yote ya dunia yanatoka ndani yao. Na wao ni sababu ya maisha ya nje yao, mahusiano yao na wanao uwezo wa kuthibiti hasira zao na tabia zao. Tabia ama hasira isiyothibitiwa hubeba wendawazimu, na mwanadamu hakuumbwa kuishi kama mwendawazimu asiye na uwezo wa kuthibiti maisha yake, na yeyote anayekasirika na kufanya shambulio lolote kwa hasira aliyoipata ni mwendawazimu, na anaishi chini ya kiwango cha uwezo wake.Amsha uwezo wa ndani leo, amsha amani ya ndani, amsha furaha ya ndani na kuwa mzuri kwa watu wanaokuzunguka hata kama hawakuvutii . Amua wewe kuwa mzuri kutoka ndani kutokana na yale unayoyafanya - na dunia yako na watu wanaokuzunguka watabadilika vivyo hivyo.MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA.Tenganamba School of life-TSL
Dar es Salaam,Tanzania.
No comments:
Post a Comment