NAIJUTIA NDOA YANGU...SEHEMU YA KWANZA

Ilikuwa kama ndoto kuolewa na mtoto wa waziri mkuu. Benson Mkama. Siku ya harusi ilikuwa ni balaa. Nilikuwa na furaha isiyo kifani. Nilijua kuwa umaskini sasa basi. Padri akasema
"Benson Mkama, unamkubali Jackline Stephano kuwa mke wako, katika shida na raha; katika hali zote mpaka kifo kitakapowatenganisha?"
Benson akajibu kwa kujiamini ;
"Ndiyo ninamkubali"
Nilitamani kuruka angani. Furaha yangu ilizidi uwezo wa kuimudu. Machozi yalianza kumiminika kutoka machoni mwangu kama chemu chemu ya maji mlimani. Ni furaha. Ni raha. Mama yangu ambaye alikuwa amesimama; kwa mshangao. Bado hakuamini kilichokuwa kinatokea. Alitoa kilio cha furaha; kilichofanya wamama wenzake wamshike. Ukweli katika familia yetu tulihisi kana kwamba tumetembelewa na Mungu live live. Mtoto wa mkulima, maskini wa kutupwa kuolewa na mtoto wa waziri mkuu; ilikuwa ni muujiza mkubwa wa karne. Ilipofika zamu yangu padri akaniuliza
"Jackline Stephano, unamkubali Benson mkama kuwa mume wako katika shida na raha, katika hali zote mpaka kifo kitakapowatenganisha?"
Nikajibu kwa sauti ya raha
"Ndiyo ninamkubali".
Padri akasema "kwasasa Benson Mkapa na Jackline Stephano ni mke na mume". Sikutaka kusikia maneno zaidi ya hayo. Maneno yake; yalikuwa kama tangazo kwa watu wote kuwa umaskini sasa kwaheri. Ndoa yangu, ilikuwa ni kukimbia umaskini wangu. Nilikuwa nimechoka umaskini na mateso.
Baada ya padri kutufungisha ndoa; tulienda mpaka ofisini kwake. Na kusaini vyeti vyetu vya ndoa. Sikuamini macho yangu sasa nimekuwa Mrs. Ben.
Siku ya harusi; viongozi wakubwa wa serikali walikuwepo. Mhe. Rais na mke wake. Magari yaliyokuwa yamepangwa nje ya kanisa la St. Joseph, yalikuwa ni mengi zaidi ya show room. Tulipoanza kutoka nje ya kanisa tulipokelewa na vuvuzela, tarumbeta,filimbi,ngoma na muziki mzito. Nilitamani nianze kucheza. Tuliingia garini na safari ya kuelekea ukumbini Mlimani city ilianza. Msafara wetu ulikuwa ni kiboko. Daladala zote na magari mengine; yalitupisha. Nilipoziona daladala nikakumbuka nilikotoka; na kujisemea kwaheri daladala, sintarudi tena huko..muda wa kula mema ya dunia umefika.
Tulifika mpaka mlimani city, ukumbi ulikuwa umepambwa nje na ndani. Tuliingia ndani ya ukumbi. Nilihisi nipo ahera. Marafiki zangu, Jane Mbise, Monalisa John na watu wengine walikuwa wanaimba
'anameremeta..dada Jack anameremetaaaa...anameremetaaaa'
Nilishindwa kujizuia. Ilinilazimu kucheza. Furaha ilikuwa imenizidi kimo. Benson naye; alijikuta anatikisa mwili wake bila kujijua. Tulipelekwa mpaka viti vya mbele; kabla ya kukaa MC ambaye alikuwa ni mtangazaji maarufu wa Clouds TV MC Kileo; akasema; haturuhusiwi kakaa mpaka tufungulie muziki kwanza. Ilikuwa ni balaa. Wimbo ukaanza kupigwa NIMEKUCHAGUA WEWE ....Ni safari ndefu ya mwanadamu....... Nywele zangu zilinisimama. Nikahisi kana kwamba roho mtakatifu ameshuka. Benson akanishika mkono. Nilijisogeza kwa kudeka; na kuanza kutikisa mwili wangu polepole na kwa maringo. Dunia ilikuwa ni yangu. Tulicheza kwa dakika mbili na kuruhusiwa kukaa. Baada ya kukaa; MC akasema huu ni muda wa kutambulisha wageni. Benson alitambulisha ndugu zake wote. Pamoja na viongozi wakubwa wa serikali. Huwezi kuamini hata Mhe. Rais alikuwepo.
Ilipofika zamu yangu; nilimtambulisha mama yangu, baba yangu wa kambo, shangazi yangu na rafiki zangu. Ambao wote walikuja kutoka mbeya. Baada ya utambulisho, nilikaa chini huku nahema kama mtu aliyekuwa anakimbizwa na mbwa; Benson akaniambia "Usipaniki mama". Nikamjibu kwa tabasamu. Waliitwa wanamziki maarufu; wakaimba. Watu wakafurahi. Kilichofuata ilikuwa ni kukata keki; ilikuwa kubwa yenye mwonekano wa sura zetu.
Sikuamini macho yangu. Tukaambiwa tusimame. Tulisimama; na kuisogelea keki huku tumeshikana mikono kama mapacha waliozaliwa siku moja. Tukapewa kisu kilichopambwa maua. Mimi na mume wangu tulikata keki vipande viwili. Nusu kipande; yenye sura ya Ben ilichukuliwa na Ben. Na nusu kipande yenye sura ya kwangu; ilichukuliwa na mimi. Benson alitembea na kuipeleka upande wa wazazi wangu. Na mimi nilitembea kwa magoti na kuipeleka upande wa wazazi wa Benson. Nilipokelewa na waziri mkuu Mhe. Aikael Mkama pamoja na mama Eda mkama. Sikuamini macho yangu. Nilijiambia moyoni; Mungu kama hii ni ndoto basi naomba nisiamke.
Baada ya kitendo hicho. Watu wote wakasimama; na kuanza kuimba ...Mungu abariki Jack na Benson...Mungu abariki Jack na Benson wape baraka na neema nyingi wadumu katikaaa ndoa yaooooo
Sikujua kwanini watu wamesimama. Nilipogeuka nyuma; nilishangaa kuona keki nyingine yenye rangi nyekundu na sura ya upendo iliyokuwa imefichwa. Ikiwa imebebwa na wazazi wetu wa pande zote mbili. Hii ilinipa shida kidogo. Benson aliipokea na kunishika mkono, na kuiweka mezani. Akainua kisu chake na kuikata katikati. Kisha akachukua kipande kidogo na kunilisha na kusema ninakupa upendo huu..kama zawadi yangu kwako itunze ndani ya moyo wako siku zote za maisha yetu. Kulingana na maelekezo ya MC.
Ilipofika zamu yangu nilichukua kipande kikubwa na kumlisha Benson na kusema ; ninakupa upendo huu..kama zawadi yangu kwako itunze ndani ya moyo wako siku zote za maisha yetu. Benson alinikumbatia na kunibusu. Baada ya hapo alinishika mkono na kuniongoza upande wa meza yetu. Tulikaa huku tumeshikana mikono. Nilitamani siku hiyo isiishe. Furaha yangu ilinifanya nisahau matatizo niliyoyapitia na kafara ya rafiki yangu Jackline niliyoitoa ili niolewe na Benson. Niliamini ndoa yangu itakuwa mwisho wa matatizo yangu. Kila mtu alisema Jackline ana bahati, lakini wengi hawakujua siri iliyonifikisha hapo.
Muda wa zawadi ulipofika; sikuamini macho yangu. Waziri mkuu Mhe. Aikael alisimama na kunipa zawadi aina ya Toyota vitz. Sikujua mbele yangu nitakutana na nini. Mazuri ya mwanzoni ya harusi yetu yalinipumbaza nikaamini kuwa ndoa yetu itakuwa ni ya raha mstarehe. Mama mkwe wangu alisimama na kutaja zawadi ya duka la nguo lililopo maeneo ya Afrikana-Mbezi beach; na kusema kuwa kwasasa nitakuwa msimamizi na mmiliki wa duka hilo. Mawifi na shemeji zangu nao hawakuwa nyuma; kila mtu alileta zawadi zake..simu, saa, tv, laptop, mafuta. Zawadi zilijaa kama duka mpya limefunguliwa. Sikujua nyuma ya zawadi hizo zimebeba nini....
ITAENDELEA SIKU YA JUMATATU...USIKOSE KILA JUMATATU
TSL Books-Geophrey Tenganamba
No comments:
Post a Comment